KKKT SASA KUWEKEZA DODOMA

Kanisa La Kiinjili La Kilutheri Tanzania Yajipanga Kuwekeza Dodoma





























KANISA la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) limesema linajipanga kuwekeza mkoani Dodoma ili kuitikia mwito wa Serikali wa kuomba wadau kujitokeza kuwekeza katika mkoa huo ambao ni makao makuu ya nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameahidi kulinunulia kanisa hilo kiwanja.

Pia kanisa hilo limetoa Sh milioni 240 kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 na mkoani Kagera.

Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Fredrick Shoo alisema hayo jana wakati wa mkutano wa wachungaji na maaskofu wa kanisa hilo unaofanyika mjini Dodoma.

Alisema kuhamia kwa makao makuu Dodoma ni azma ya serikali na kanisa la Kilutheri lina nia na linahitaji kuwa na eneo la makao makuu ili kuweza kuendeleza taasisi zao. Alisema kanisa hilo linajipanga ili kuwekeza Dodoma baada ya ardhi kupatikana.

Alimuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliyekuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kufungua mkutano huo kusaidia kanisa hilo wakati wa kuuzwa kwa viwanja, kanisa hilo likumbukwe.

“Nimepokea hilo nitashirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha maeneo yanapatikana,” alisema Mwigulu.

Pia alisema kutokana na kulelewa na Umoja wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (Ukwata) akiwa mwanafunzi, zawadi yake kwao ni kuwatafutia kiwanja Dodoma.

“Nitanunua kiwanja hicho kwa gharama zangu na nitawakabidhi na nilifanya hivyo mkoa wa Pwani na sasa wanakaribia kukabidhiwa hati,” alisema.

Mwigulu alitoa sadaka ya Sh milioni tano.

#habarileo.co.tz

Comments